KANALI MUAMMAR GADDAFI (1942 - 2011).

SEHEMU YA PILI
Licha ya Gaddafi kufanikiwa sana katika kuboresha hali za kimaisha za wananchi wake lakini pia alijikita sana kutaka kuunganisha nchi zote za kiarabu zilizoko kaskazini kwa afrika na mashariki ya kati.
Maono ya Gaddafi yalikuwa ni kuona mataifa ya kiarabu yanaungana na kutengeneza taifa moja lenye nguvu kubwa.
Alifanikiwa kushawishi Marais wa Misri na Syria kuungana naye katika mpango huu.
Kutokana na uchumi wa Libya kuimarika kwa kasi kutokana na usimamizi mzuri wa mapato ya makubwa yatokanayo na uchimbaji mafuta, Gaddafi alitimia pia uwezo huu wa kiuchumi kushawishi mataifa maengine kuungana naye katika agenda zake.
Kwa mfano nchi za kiarabu zilizounga mkono maono yake ya kuwa na taifa moja la Kiarabu alizipatia msaada mkubwa wa kifedha.
Nchi hizo zilikuwa ni Misri, Sudan, Syria na Iraq.
Maono ya kuwa na taifa moja la Kiarabu yalivirugika mno kutokana na kifo cha ghafla cha 'mentor' wake Rais wa Misri Nasser.
Aliyekuja kumrithi Nasser, rais mpya wa Misri Anwar Sadat mwanzoni alionyesha muelekeo mzuri wa kuunga mkono maono ya kuwa na nchi moja ya Kiarabu.
Hii ilidhihirishwa pia n kuwahi kusainiwa kwa makubaliano ya mashirikiano kwa kuunda shirikisho la nchi za kiarabu ambalo walilita Union Of Arab Republics.
Mkataba huu ulisainiwa na Gaddafi, Rais Anwar Sadat wa Misri na Rais Hafez Al-Assad wa Syria.
Lakini baadae Rais Anwar Sadat wa Misri akaanza kujitenga na ushirikiano huu akidai kuwa anaogopeshwa na msimamo mkali wa Gaddafi.
Lakini Gaddafi alimtuhumu kuwa Anwar Sadat amegeuzwa kuwa kibaraka wa magharibi.
Pia Gaddafi alikasirishwa mno na kitendo cha NATO kuwa na kituo cha kijeshi katika Kisiwa cha Malta eneo la Mediterranean. Kitendo hiki alikiona kama hatari kubwa kwa nchi za kiarabu na pia alitafsiri kama chokochoko kutoka kwa nchi za kimagharibi.
Hivyo basi akamshawishi Rais wa Kisiwa cha Malta wa kipindi hicho Dom Mintoff kukataa kuendelea kwa shughuli za NATO katika Kisiwa chao.
Gaddafi hakumshawishi Dom Mintoff hivi hivi tu, bali alitengeneza ihusiano wa karibu sana baina ya nchi hizo mbili na pia akimimina misaada lukuki ya kifedha kwenda Malta.
Mwanzoni Malta waliogopa kuwafukuza NATO kama bavyo Gaddafi alitaka, walichokifanya wakawaruhusu NATO waendelee kuweka kituo cha kijeshi kisiwani mwao lakini kwa sharti kwamba kituo hicho kamwe kisije kutumia kuanzisha mashambulizi kwa nchi za kiarabu.
Gaddafi hakukata tamaa aliendelea kumimina misaada kwenda Kisiwa cha Malta na kuimarisha uhusiano wao na hatimaye mwaka 1980 mkataba wa kwanza wa miaka kumi kati ya Malta na NATO ulipoisha, Malta kwa ushawishi mkubwa wa Gaddafi wakakataa kusaini mkataba mpya wa kuiwezesha NATO kuwela kituo cha kijeshi.
Gaddafi hakuishia hapo tu katika kuwaonyesha 'jeuri' mataifa ya magharibi.
Alaanzisha mpango kabambe wa kununua ndege na silaha za kivita kutoka Urusi.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi hiki, ndipo ambapo Vita baridi kati ya Marekani na Urusi vilikuwa vimepamba moto. Hivyo kitendo cha Gaddafi kujenga mahusiano ya karibu ya kijeshi kiasi hiki kiwaudhi mno wa magharibi na moja kwa moja wakamtafsiri kama mtu hatari kwao.
Pia Ghaddafi aliipinga vikali Marekani juu ya msimamo wake wa kuunga mkono Israel kwa kitendo chao cha kukalia ardhi ya Palestrina.
Gaddafi aliamini kwamba Israel ilikuwa ni mkakati wa nchi za magharibi kuleta ukoloni kwa nchi za kiarabu.
Gaddafi akachochea uanzishwa wa mfuko wa jihad (Jihad Fund) ambao ulisaidia kuanzishwa kwa kituo cha Nasserite Volunteers Center ambacho kilitoa mafunzo kwa wapiganaji wa kijeshi walioipinga Israel.
Muammar Gaddafi, Rais Hafez Al-Assad na Rais Anwar Sadat wakisaini makubaliano ya "Union Of Arab Republics"
Baadae Gaddafi kama ilivyokuwa kwa 'mentor' wake Nasser akaanza kumuunga mkono kwa nguvu Yasser Arafat na kikundi chake cha Fatah.
Lakini kadiri miaka ilivyosonga, uhusiano kati ya Gadaffi na Yasser Arafat ulizidi kuzorota, Gaddafi akidai kwamba Arafat amekuwa "mwanasiasa" na amepoa mno (too moderate) na badala yake akaanza kuunga mkono vikundi vya wapiganaji kama vile Popular Front for the Liberation of Palestinepamoja na vikundi vingine vya wapiganaji wa kijeshi.
Gaddafi pia alifadhili kikundi cha Black September ambacho kilihusika kufanya shambulizi dhidi ya wanamichezo wa Israel nchini Ujerumani. Gaddafi alifika mbali zaidi, hata kusafirisha miili ya wapiganaji waliouwawa katika mapambano yale mpaka Libya na kuwapa mazishi ya kishujaa wapiganaji hao wa Kipalestina.
Kiufupi Gaddafi alifadhili vikundi vingi vya wapiganaji duniani kote walioonyesha dalili ya kupinga nchi za kimagharibi.
Alifadhili vikundi kuanzia mashariki ya kati, Amerika ya kusini, ufilipino, Eritrea, Gabon, CAR mpaka afrika ya kusini ambako alikifadhili kikundi cha ANC kilichokuwa kinapambana na serikali na utawala wa kibaguzi nchini humo.
Kitendo hiki kilimjengea sifa kubwa ya kuonekana kama kiongozi Mkuu wa wazalendo wa ulimwengu wa tatu wanaopinga ukoloni na ukoloni mamboleo.
Lakini mataifa ya magharibi waliona Picha ya tofauti. Walimuona Gaddafi kama mfadhili wa "ugaidi" duniani. Walimuona kama tishio na kikwazo katik a mikakati yao ya kujipenyeza kwenye nchi za ulimwengu wa tatu na nchi za kiarabu.
Kwahiyo wa magharibi hawakujali kwanini Gaddafi alikuwa na misimamo aliyokuwa nayo, misimamo ambayo muda mwingine Gaddafi ilimbidi tu kuwa nayo ili aweze kuwapinga mataifa ya magharibi kwa sera zao kandamizi.
Licha ya mapungufu ambayo Gaddafi alikuwa nayo kama binadamu mwingine na pia muda mwingine akitumia madaraka yake vibaya au hata kunyanyasa au 'kuwapoteza' waliompinga, lakini historia ya dunia haitatenda haki kwa kutokukiri kwamba Gaddafi ni moja ya viongozi mahiri kuwahi kutokea duniani na mzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake na nchi zote za ulimwengu wa tatu.
Ushahidi huu hauwezi kuupata katika makala au vyombo vya habari ya kimagharibi ambao wametumia umahiri mwingi kumpaka matope Gaddafi na kimjengea Picha ya kuonekana kama 'kituko' au gaidi.
Ukitaka kupata uhalisia wa umahiri wa Gaddafi na uzalendo wake, itazame historia na zitazame namba… wanasema namba hazidanganyi.
Mwaka 1969 Gaddafi alipokea kutoka kwa Idris, nchi ya Libya ikiwa moja kati ya mataifa masikini zaidi duniani.
Mpaka kufikia mwaka 2011 alikuwa amefanikiwa kuifanya Libya taifa tajiri zaidi Africa likiongoza kwa GDP. Pia Libya ilikuwa na watu wachache zaidi wanaoishi chini ya mstari wa umasikini kuishinda hata nchi ya uholanzi.
Nieleze pia 'maajabu' machache mengine ambayo Gaddafi aliyafanya kwa nchi yake mpaka kufikia 2011;
- Gaddafi aliifanya familia kuwa na nyumba nchini Libya ni Haki ya Binadamu. Kwamba kila familia ni lazima iwe na makazi. Hili amelieleza vyema sana kwenye kitabu chake cha The Green Book. Na alihakikisha kwamba serikali yake inaipatia nyimba kila familia.
- Elimu ilikuwa inatolewa bure nchini Libya kuanzia msingi mpaka Chuo Kikuu.
- katika utawala wa Gaddafi Libya ndiyo ilikuwa nchi yenye kutoa huduma bora zaidi za kiafya barani Afrika na huduma hii ilitolewa bure kwa watu wake. Pia wananchi ambao walitakiwa labda kupata matibabu fulani nje ya nchi, walilipiwa na serikali.
- serikali ya Gaddafi ndiyo iliyotekeleza mradi mkubwa zaidi wa kilimo cha umwaguliaji kwenye historia ya Dunia. Hii ilihusisha kutengeneza mto ambao ulitembea nchi nzima. Gaddafi mwenyewe alipenda kuita mradi huu kama "ajabu la nane la dunia."
- mwananchi wa Libya alikuwa akitaka kuanzisha mradi wa kilimo, anapewa nyumba, shamba, mifugo na mbegu za kuanzia. Vyote hivi anapewa bure na serikali ya Gaddafi.
- chini ya serikali ya Gaddafi, mama mjamzito akijifungua alikuwa anapewa dola elfu tano (zaidi ya milioni kumi ya Tanzania) kwa ajili yake na mtoto.
- chini ya Gaddafi, umeme ilikuwa bure nchini Libya.
- kipindi cha Gaddafi, bei ya mafuta ya gari kwa wananchi nchini Libya ilikuwa chini mpaka kufikia dola 0.14.
- wakati Gaddafi anaingia madarakani ni wananchi 25% walikuwa wameelika lakini mpaka kufikia mwaka 2011 zaidi ya 87% ya wananchi walikuwa na elimu.
Haya ni machache kati ya 'maajabu' Mengi mno ambayo Gaddafi aliyafanya kwa watu wake na kuibadilisha na kuipaisha Libya.
Lakini wapo watu ambao maslahi yao yaliguswa… na wakajiapiza lazima "gaidi" huyu aondoke…
Katika sehemu itakayofuata niateleza kuhusu mkakati wa kipropaganda na kijeshi na hatua kwa hatua namna Gaddafi alivyoondolewa.
KUPAA NA KUTUNGULIWA
Katika sehemu iliyopota nilijaribu kueleza japo kwa uchache ni kwa kiasi gani ambavyo Gaddafi kama kiongozi wa Libya, alifanikiwa kuibadilisha nchi kutoka kwenye kundi la nchi masikini zaidi na kuifanya moja ya nchi zenye GDP kubwa zaidi.
Nilieleza japo japo kwa uchache mafanikio ambayo Gaddafi aliyapata na kubadili hali za maisha za watu wa Libya.
Katika sehemu hii ya tano ya makala hii ningependa kueleza kwa kirefu namna ambavyo Gaddafi aliondolewa madarakani na hatimaye kuuwawa na wananchi wake mwenyewe kwa msaada mkubwa wa uchochezi na uongozi wa nchi za Magharibi kinara akiwa Marekani.
VUGU VUGU LA MAPINDUZI KATIKA NCHI ZA KIARABU
Baada mahangaiko ya miaka mingi kutafuta ajira bila mafanikio pamoja na manyanyaso ya muda mrefu kutoka kwa askari wa manispaa ya mji wa Sidi Bouzid, nchini Tunisia, hatimaye siku ya tarehe 17 mwezu desemba mwaka 2010 saa tano na nusu asubuhi, kijana Mohamed Bouaziz alijichoma moto nje ya ofisi ya Havana kuonyesha uchungu alionao dhidi ya serikali ya Rais Zine El Abidine Ben Ali.
Kitendo hiki kulikuwa sawa kumwagia mafuta ya taa katika moto uliokuwa unawaka chini kwa chini. Hii ilipelekea kuwa mwanza wa maandamano makali ambayo yalisababisha Rais wa Tunisia Ben Ali kujiuzuru tarehe 14 January 2011, baada ya kutawala nchi ya Tunisia kwa miaka 23.
Wimbi hili la hasira za wananchi kutaka mabadiliko halikuishia Tunisia pekee bali likaenea katika nchi tano nyingine za kiarabu ambazo athari za vuguvugu hili ilikuwa ni kubwa sana. Nchi hizo ni Libya, Misri, Yemen, Syria na Iraq.
Lakini pia kulikuwa na nchi nyingine kadhaa za kiarabu ambazo pia vugu vugu japokuwa hakukuwa na athari kubwa sana kama nchi tano nilizozoitaja awali lakini nako walionja lafha ya vugu vugu hili la kudai mabadiliko. Nchi hizo ni Jordan, Oman, Iran, Morocco, Kuwait, Bahrain, Algeria, Lebanon na Sudan.
Kipindi vugu vugu hili linaanza huko Tunisia, Muammar Gaddafi akafanya kosa kubwa la kumuunga mkono wazi wazi Rais Ben Ali ambaye wananchi walikuwa wanamshinikiza aachie madaraka baada ya kuitawala Tunisia kwa miaka 23.
Kitendo hiki kiliaanza kutoa mwanya kwa wabaya wake kuanza kupenyeza propaganda kwamba Gaddafi anaunga mkono watawala "madikteta" wanaotawala nchi kana kwamba ni wafalme na anawaunga mkono kwa kuwa na yeye ni mtawala wa namna hiyo na ameitawala Libya kwa miongo minne.
Baada ya serikali ya Gaddafi kuhisi kwamba kuna joto la vugu vugu linafukuta mitaani na linaweza kulipuka dakika yoyote akachukua hatua kadhaa za tahadhari na ili kutuliza hasira za wananchi wasianzishe maandamano.
Kwanza kabisa serikali ikashusha bei ya vyakula nchi nzima.
Hii ilikiwa ni moja ya sababu za waandamanaji kuwa na hasira huko nchini Tunisia. Bei za vyakula zilikuwa juu mno katika nchi za kiarabu kaskazini mwa Africa katika kipindi hiki. Kwahiyo serikali ya Gaddafi ili kushusha hasira za wananchi akashusha bei za vyakula nchi nzima.
Pili, akaanza kulisafisha jeshi kwa kuondoa wanajeshi wote wenye vyeo vya juu ambao aliamini kuwa wanadalili hata kidogo tu ya kwamba wangeweza kuja kumsaliti.
Tatu, Gaddafi akawaachilia huru wafungwa wote wa Kiislamu ambao aliwafunga gerezani kwa kutoa mawaidha makali yenye kumkosoa. Wengi wa wafungwa hawa walikuwa wanakubalika sana kwenye jamii na walikuwa na ushawishi kwa kiwango fulani. Kwahiyo Gaddafi aliwaachia akiamini kwamba suala hilo litaleta furaha kwenye jamii na hatimaye kupooza hasira zao dhidi ya chuki iliyoanzwa kuenezwa ya kumkosanisha na wananchi wake.
Licha ya hatua hizi muhimu zilizo chukuliwa na uongozi wa Gaddafi ili kufifisha hasira za wananchi zilikuwa za bure na hazikufua dafu mara baada ya January 14, 2011 siku ambayo wananchi wa Tunisia walimng'oa madarakani Rais Ben Ali.
Hii iliwapa moyo wanaharakati waliokinyume na uongozi wa Gaddafi kuwatia moyo wananchi kwamba kilichotokea Tunisia kinaweza pia kutokea Libya ikiwa wananchi watasimama kidete.
Katika miji ya Beyda, Derna na Benghazi kulikuwa na Miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi unaendelea chini ya ufadhili wa serikali lakini ukamilishaji wa miradi hii ulikuwa umechelewa mno kwa miezi kadhaa. Wananchi walikuwa wanalalamika kwa kipindi kirefu kuwa kulikuwa na harufu ya rushwa iliyokithiri katika ujenzi wa nyumba hizo.
Kwa hiyo baada ya hasira za vugu vugu kuwaingia wananchi na mori iliyowaingia baada ya wananchi wenzao kumng'oa rais huko Tunisia, ghafla katika miji hii ya Beyda, Derna na Benghazi kukaanza kutokea maandamano ya wananchi kuonyesha hasira zao juu ya kucheleweshwa kukamilika kwa miradi hiyo na harufu ya rushwa iliyopo katika hiyo miradi.
Maandamano haya ambayo awali yalikuwa ya amani baadae yaligeuka na kuwa ya vurugu kubwa. Wananchi walivamia majengo haya ya makazi yaliyokuwa yanajengwa na kuyabomoa na kuyachoma moto mengine. Lakini pia wananchi kwenye hii miji hawakuishia hapo tu kwenye kubomoa majengo ya makazi bali pia wakaanza kuvamia ofisi za serikali na kufanya uharibifu.
Katika dhamira njema ya kuwatuliza wananchi, serikali ya Gaddafi ikatoa kiasi cha Euro bilioni 20 (zaidi ya Trilioni 45 za Kitanzania) ambazo zikawekezwa katika ujenzi zaidi wa nyumba za makazi. Gaddafi na wenzake serikalini waliamini kuwa hii ingeweza labda kurudisha tena imani ya wananchi na kuwafanya watulize hasira dhidi ya utawala wake.
Lakini hii nayo haikufua dafu, chuki ilizidi kuenezwa kwa wananchi wa Libya.
Mchambuzi maarufu wa masuala ya kisiasa nchini humo Bw. Jamal Al-Hajji akaanzisha kampenzi kupitia mitandao ya kijamii kuhamasisha wananchi kudai "Uhuru wa Kweli" wa nchi ya Libya.
Siku ya February 1, Jamal alikamatwa na maaskari kanzu akiwa Nyumbani kwake na akafunguliwa mashataka matatu.
Mwezi huo huo wa February, Gaddafi akafanya kikao maalumu na wanaharakati wa kisiasa, waandishi wa Habari na Wamiliki wa Vyombo vya habari na akawakemea vikali juu ya mwenendo wa nchi unavyokwenda na wao wakionekana ni vichochezi wakubwa katika mwenendo huo hasi wa nchi.
Pia Gaddafi akawapa onyo kwamba watawajibika ikitokea amani ya nchi ikivurugika kwa sababu yao.
'Mkwara' huu wa Gaddafi nao haukufua dafu, bado harakati za mitandaoni ziliendelea kwa kasi kubwa zaidi watu wakihamasishana kumuondoa madarakani Gaddafi na serikali yake.
Katika hali iliyoonekana kama kuunga mkono harakani hizi za mirandaoni, moja ya washauri wakuu wa Gaddafi alijiuzuru kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Joto lilipanda zaidi baada ya wananchi wa Liby a kupata habari kwamba wananchi wenzao wengine wa Misri wamefanikiwa kumuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak.
Baadae maandamano yakasambaa kwenye miji mingine zaidi kama vile Zawiya na Zintan.
Kadiri maandamano yalivyokuwa yanapamba moto kwenye miji mbali mbali kidogo kidogo yakaanza kugeuka kutoka kwenye maandamano ya amani na kuwa maandamano yenye vurugu na gasia kubwa.
Waandamanani walivamia majengo ya serikali pamoja na vituo vya polisi na kuvichoma moto.
Katika miji mingine polisi ilikuwa inawabidi kuwaunga mkono waandamanaji ili kunusuru maisha yao.

wananchi wakiwa wameandamana katika siku za mwanzo maandamano mjini Benghazi
Maandamano nchini kote Libya yalienda sambamba na kampeni za mitandaoni hasa Facebook na Twitter kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi barabarani waweze kumng'oa Gaddafi madarakani.
Pamoja na kampeni za Twitter na Facebook, pia wanamuziki kadhaa ambao awali nyimbo zao zilipigwa marufuku kutokana na maudhui ya nyimbo zao kujaa chuki dhidi ya Gaddafi, ghafla wakaanza kupata umaarufu mkubwa na nyimbo zao kutumika kama 'nyimbo za halaiki' katika maandamano.
Moja wapo ya wanaziki hao ni kijana ambaye bado hajulikani ni nani, lakini mwenyewe hupenda kujiita 'Ibn Thabit' katika tovuti yake. Kijana huyu niwanamziki wa staili ya kufoka foka (rap) na tangu mwaka 2008 alikuwa anaachia nyimbo zenye maudhui ya kukosoa utawala wa Gaddafi.
Katika kipindi hiki cha vugu vugu alitoa kibao ambao kilijipatia umaarufu mkubwa kwa waandamanaji ambacho kiliiitwa 'Al Soo'al' akiwa na maana ya 'Swali' (The Question).
Moja kati ya mstari uliokuwa unawakonga nyoyo waandamanaji ulikuwa ni huu ufuatao (katika tafsiri ya kiswahili);
"Muammar: hujawahi kuwa na dhamira ya kutumikia umma.
Muaamar: vyema ujisalimishe na kutubu. Huwezi kukimbia kisasi chetu
Kama treni linavyounguruma na kusaga ukuta, ndivyo tutakavyo kuzamisha."
Maandamano yakaendelea kuwa makali zaidi nchi nzima. Waandamanaji wakaanza kubeba mabomu ya petroli (petroli na utambi kwenye chupa) na kurusha kwenye majengo ya serikali na kuyateketeza kwa moto.
Pia mabomu haya ya petroli pamoja na mawe yalirushwa kwa askari wa kutuliza ghasia.
Baada ya maandamano kufikia hatua hii ya waandamanaji kutumia 'silaha', polisi na wanajeshi wakamwagwa mitaani kiwatuliza. Mwanzoni wakaanza kuwarushi mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
Siku za baadae kadiri fujo zilivyoongezeka wanajeshi na polisi wa kutuliza ghasia wakaanza kutumia risasi za mpira.
Baadae Gaddafi akatoa ruhusu kwa askari kutumia risasi za moto.
Hapa ndipo "mchezo uliponoga".
Kukaanza kuibuka ripoti za mamia ya waandamanaji kuuwawa na polisi pamoja na wanajeshi huko mitaani kwenye maandamano.
Hii ilipelekea viongozi wengi serikalini kujiuzuru kama hatua ya kupinga uamuzi huu wa kuruhusu wanajeshi na polisi kutumia silaha za moto dhidi ya wananchi.
Hali hii ya waandamanaji kuuwawa badala ya kuwatisha wananchi, badala yake iliwafanya kuwa kama vichaa. Hasira zao zilizidi maradufu na wakazidi kufanya maandamano ya ghasia kubwa zaidi wakiteka vituo vya redio na kuvamia majengo ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Hii ilipelekea tarehe 18 February wanajeshi wote na polisi kukimbia mji wa Benghazi baada ya kuzidiwa nguvu na wananchi.
Hii inaakisi uzuri na udhaifu wa moja ya mbinu mujarabu kabisa ambayo Gaddafi alikuwa akiitumia kwa miaka mingi kwaafanikio makubwa lakini ilikuja kumgharimu katika kipindi hiki cha vugu vugu la maandamano ya wananchi kutaka ang'oke madarakani.
Tukumbuke kwamba Gaddafi aliingia madarakani kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi, hivyo alikuwa na ufahamu wa kutosha juu ya hatari ya jeshi kwa kiongozi wa nchi (mapinduzi).
Hivyo basi kwa miaka yote ya utawala wake, kwa makusudi kabisa, alihakikisha Libya ina jeshi dogo (kwa idadi ya watu). Mfano wanajeshi wote wa Libya walikuwa hawazidi 50,000.
Lakini pia katika ngazi za juu za uongozi wa kijeshi aliwaweka watu ambao anajua kuwa wanamuunga mokono kwa dhati kabisa. Yaani watoto wake, ndugu na watu kutokea kabila lake.
Pia jeshi lote la Libya aliliunda katika namna ambayo lilikuwa na brigedia nne tu ambazo zilikuwa na wanajeshi wenye weledi naafunzo ya hali ya juu ya kijeshi na vifaa vya kisasa. Mfano, moja ya brigedia hizo nne iliitwa Khamis Brigade na iliongozwa na mtoto wake aliyeitwa Khamis.
Suala hili la kuwa na jeshi dogo na kuwa na brigedia chache zenye mafunzi ya weledi na vifaa vya kisasa lilimsaidia kuepuka kullpinduliwa na jeshi kwa zaidi ya miongo minne lakini lilimgharimu sana katika kipindi hiki.
Katika sehemu ya tatu nitaeleza namna ambayo vikundi vya wapiganaji waasi vilivyoibuka na kufanikiwa kumuondo a madarakani Gaddafi na hatimaye kumuua kama mnyama.
Comments
Post a Comment