KANALI MUAMMAR GADDAFI (1942 - 2011)

SEHEMU YA TATU


Moja ya michoro ya kumkejeli Gaddafi iliyochorwa mjini Bayda baada ya vurugu kushika kasi nchi nzima

Katika sehemu iliyopita nilieleza namna ambavyo vugu vugu la maandamano jinsi lilivyoibuka na kukolea katikati mwa mwezi February mwaka 2011.

Katika sehemu hii ya tatu nakusudia kuandika zaidi kuhusu namna ambavyo vikundi vya waasi viliibuka na hatimaye kumuondoa Gaddafi madarakani.

Tuendelee…
Baada ya vugu vugu kupamba moto hasa na maandamano kukolea karibia nchi nzima ya Libya, na hatimaye kundi kubwa la polisi na wanajeshi kuasi, taratibu ikaanza vugu vugu la kupinga Gaddafi kwa kutumia silaha badala ya maandamano pekee.

Mwanzoni kabisa mwa vugu vugu hili la kutumia silaha, vikundi vya wapiganaji vilikuwa vinaundwa na raia wa kawaida waliojitolea kushika mtutu.
'Volunteers' hawa waliojitolea kupigana walikuwa wengi wao wanatoka kada za ualimu, wanafunzi, na wafanyakazi katika visima vya mafuta.
Taratibu wanajeshi na polisi wakaanza kujiunga nao na kukoleza moto wa kumoinga Gaddafi kwa mtutu wa bunduki.

Mpango huu (kumpinga Gaddafi kwa silaha) ulikuwa ni mtego mujarabu kabisa wa mataifa ya magharibi ambao waliusuka kwa umakini ili wamuingize Gaddafi ajikaange mwenyewe na pasipo kujua au labda kutokana na kupaniki kutokana vurugu zilizokuwa zinaendelea nchi nzima Gaddafi akajiingiza kwenye mtego.

Kwanini nasema huu ulikuwa ni mtego?

Mara zote mataifa ya magharibi wakiongozwa na Marekani huvamia nchi kwa kisingizio cha kulinda amani au kulinda raia ikitokea serikali ya nchi husika ikianza kutumia jeshi kudhuru raia wake.

Kwa hiyo muitikio wa kijeshi wa Gaddafi baada ya raia wakorofi kuanzisha vugu vugu la kutumia silaha ulikuwa ni mwanya muafaka kwa mataifa ya magharibi kujipenyeza na kutekeleza mkakati wao wa kijeshi.

Vugu vugu hasa la raia kutumia silaha lilishika kasi kuanzia tarehe 17 February 2011.
Baada ya vugu vugu hili la kutumia silaha kupamba moto ndipo hapa napo hata vikundi vingi vya wapiganaji wa kiislamu wenye msimamo mkali vilivyokuwepo miaka yote navyo vikatumia hii fursa kufanya harakati zao kwa mgongo wa kudai mapinduzi na kumuondoa madarakani Muammar Gaddafi.

Mfano katika mji wa Benghazi, vikundi 12 vya kiislamu viliungana na kulinda umoja waliouita "The February 17th Brigade".
Huko mji wa Misrata na Zaria kukaibuka kikundi cha wapiganaji waliojiita "The Libya Shield".

Kwenye miji ya Zatan na Derna kukaibuka kikundi cha kiislamu cha "Libyan Islamic Fighting Group".

Lakini pia kulikuwa na vikundi vingine kama vile "Obaida Ibn Jarrah" na kadhalika.

Moja ya michoro ya kumkejeli Gaddafi iliyochorwa mjini Bayda baada ya vurugu kushika kasi nchi nzima
Serikali ya Gaddafi mara kadhaa ilijaribu kujenga hoja kwa jamii ya kimataifa kwamba vikundi hivi vingi vilikuwa na chembe chembe za mawakala wa kikundi cha kigaidi cha Al Qaida lakini vikundi vyenywe vya waasi walikuwa wanakanusha vikali suala hili.

Lakini kuna wakati ambao kamanda mkuu wa vikosi vyote vya NATO, kamanda James G. Stavridis aliwahi kukiri kwamba kwa kadiri ya taarifa za intelijensia ambazo NATO walikuwanazo, walikuwa wanaamini kwamba kulikuwa na uwezekano wa vikundi hivi vya wapiganaji kuwa na mawakala wa kikundi cha Al Qaida.

Lakini kamanda Stavridis akajenga hoja kwamba uwepo wa wanachama hao wa Al Qaida bado hauna ushahidi wa kutosha kuweza kuthibitosha pasina shaka na hadhani kama kujipenyeza kwao kwenye vikundi hivi vya wapiganaji wa Libya waliokuwa wanataka kufanya mapinduzi ya kumuondoa Gaddafi hakudhani kama walikuwa na ushawishi wowote wa kuweza kuathiri mwenendo au misimamo au muelekeo wa vikundi hivi.

Lakini hoja hizi za Kamanda Stavridis hazina ukweli au labda tuseme zina ukweli nusu tu.
Kuna mawasiliano ya siri ya kieletroniki yaliyonaswa ambayo yalitimwa kutoka ubalozi wa Marekani uliopo Tripoli kwenda kituo cha Combating Terrorism Center katika kituo cha kijeshi cha Marekani kilichopo West Point, ambapo mawasiliano haya yanaonyesha kuwa Marekani walikuwa na taarifa thabiti kabisa kwamba moja wapo ya viongozi wa vikundi vya wapiganaji wanaodai mapinduzi kumuondoa Gaddafi, ambaye aliitwa Abu Sufian Ibrahim Ahmed Hamuda Bin Qumu ambaye kwa wakati huu ulikuwa ni kiongozi wa kikundi cha wapiganaji wabaodai mapinduzi wa Libyan Islamic Fighting Group aliwahi kujiunga na wapiganaji wa Taliban huko nchini Afghanistan mwaka 1998.

Pia Abu Sufian Qumu aliwahi kuwa mfungwa katika gereza la Marekani la Guantanamo Bay.

Pia mawasiliano haya ya siri yalikuwa yanajaribu kutahafharisha jeshi la Marekani kuwa yawezakana Abu Sufian Qumu alikuwa na mafungamano na Al Qaida na pia yawezekana alikuwa ni mwanachama wa African Extremist Network.

Kutokana na vurugu zilizokuwa zinaendelea nchi nzima Gaddafi zilimpandisha hasira Gaddafi na akaapa kamwe hawezi kuachia madaraka kwa sababu ya vugu vugu ambalo alikuwa na hakika lilikuwa linaratibiwa kwa siri kubwa na mataifa ya magharibi.
Hivyo basi Gaddafi akaapa kuwasaka wapiganaji wa vikundi vinavyompinga pamoja na wanaowaunga mkono ambapo alijiapiza kwa kauli ambayo ilijipatia umaarufu sana, kwamba atawasaka "mtaa kwa mtaa, nyimba kwa nyumba na kabati kwa kabati."

Gaddafi pia akawabatiza jina waasi kuwa ni "cockroaches" na "rats"!

Ili kuonyesha kwamba hakuwa anatania alichokuwa anakisema, Gaddafi alilihutubia taifa na kusema kuwa anapokea simu za maelfu ya wananchi kutoka Benghazi wanaodai kuwa wametekwa na kuzuiwa kutoka majumbani kwao kama mateka.

Hivyo Gaddafi akatoa rai kwa vikundi vya wapiganaji kuwa wote ambao watajisalimisha au kutuma silaha na kurejea kwenye maisha yao ya kawaida watasamehewa, lakini wale wote ambao warakaidi agizo hilo, kitakacho wapata damu yao itakuwa juu yao wenyewe.

Hii ilikuwa inakaribia mwishoni mwa mwezi February, na baada ya kauli hizi kali kutoka pande zote mbili ndipo hapa hasa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya ikaanza.!!


KIFO CHA MUAMMAR GADDAFI


Moja ya vikao vya kwanza kabisa vya vikundi vya upinzani mjini Bayda vilivyopelekea kuundwa kwa National Transitional Council

Yako mengi ningeweza kuandika kuhusu mapigano ya vikosi vya jeshi vitiifu kwa Gaddafi dhidi ya vikundi vya kudai mapinduzi na kumuondoa Gaddafi madarakani. Lakini nisingependa niandike sana kwa leo kuhusu mapigano hayo badala yake nataka kuegemea zaidi kwenye mfululizo wa matukio ya mwishoni mwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yalipelekea kuuwawa kwa Gaddafi.

Tuendelee…

Mwishoni mwa mwezi February (tarehe 27), kukajitokeza muungano wa kisiasa wa vikundi vyote vya wapiganaji ambao wakaunda ummoja amabo waliufanya kama chombo chao cha uwakilishi wa kisiasa.
Umoja huu waliuita National Transitional Council (NTC).

NTC ilijipambanua kama ndio wawakilishi rasmi wa watu na taifa la Libya.

Mwezi March NTC wakatangaza kutoitambua serikali ya Gaddafi na kujitangaza wao kuwa ndio chombo halali chenye mamlaka ya kutawala na kiserikali nchini Libya.

Kutokana na mataiafa ya magharibi kumpinga vikali Gaddafi haikuchukua muda wakaanza kuitambua rasmi NTC kama chombo cha kimamlaka na kiserikali kwa niaba ya Libya.
Hatua hii ya kuitambua NTC kama chombo rasmi chenye mamlaka 'halali' nchini Libya, ilienda sambamba na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuamuru ku-freeze mali zote za Gaddafi kila sehemu zilipo duniani. Kuanzia fedha kwenye mabenki ya nje mpaka mali zisizohamishika.
Na si hivyo tu, ili pia kuzuia Gaddafi na washirika wake wa karibu wasiweze kutoroka kwenda nje ya nchi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ukalifanya anga lote la Libya kuwa ni "No fly zone" na wakatoa kibali kwa vikosi vya NATO kutumia nguvu zote walizonazo kuwasaidia NTC kumuondoa madarakani Gaddafi kwa kisingizio kwamba serikali yake ilikuwa inatekeleza oparesheni zenye kukiuka haki za binadamu kwa kiwango kikubwa na kudhalilisha utu wa binadamu.

******

Mwanzoni mwa vita hii vikosi vya Gaddafi zilionyesha kila dalili ya kuwashinda vikundi vya waasi wa NTC.
Lakini baadae kibao kikageuka hasa baada ya NTC kuanza kupata usaidizi kutoka kwa Marekani na washirika wake.

Taratibu vikosi vya NTC vikaanza kuchukukua mji mmoja baada ya mwingine na kuiweka kwenye himaya yake.

Vikosi vya waasi vilifanya mashambulizi makubwa mpaka kufanikiwa kuutwaa mji mkuu wa Tripoli. Walipofikia kuutwaa mji huu ilibidi Gaddafi atoroke na kukimbilia maeneo ya kusini mwa Libya.

Gaddafi aliotoroka Tripoli na msafara Mdogo sana wa magari ili asiweze kugundulia na akaelekea Sirte.
Mtoto wake Mutassim Gaddafi alimfuata baadae akiwa na msafara mwingine wa magari.
Akiwa Sirte Gaddafi alijificha ndani ya mji huo kwa miezi kadhaa akiwa na ulinzi mkali wa vikosi vyenye silaha nzito.

Vikosi vya waasi vilizidi kusonga mbele ambapo karibia na mwezi September walifanikiwa kuuteka mji wa Bani Walid ambao ulikuwa na wakazi wengi wenye kumuunga mkono Gaddafi.

Baadae mwanzoni mwa mwezi October waasi wakaanza kuinyesha dalili za kufanikiwa kuutwaa mji wa Sirte.

Wasaidizi wa karibu wa Gaddafi akiwemo Mansour Dhao kiongozi wake wa vikosi vya "People's Guard" ambaye alikuwa pamoja na Gaddafi mafichonj ndani ya mji wa Sirte anadai kwamba ilifika kipindi Gaddafi akawa "anaishi nje ya uhalisia".
Mfano wakuu wake wote wa masuala ya ulinzi walikuwa wanamshauri kuwa watoroke kwenda nchi jirani, lakini Gaddafi alikataa kata kata kuwa hawezi kuondoka Libya.



Mapigano ya kugombea mji wa Sirte kati ya wapiganaji wa NTC na jeshi la Gaddafi

Baada ya vikosi vya wapiganaji wa NTC kuzidi kusonga mbele na kuuchukua zaidi mji wa Sirte, Gaddafi akafanya kosa kubwa la kutaka kutoroka kutoka mji huu.
Au pengine niseme kosa lake kubwa lilikuwa ni kuondoka wote kwa pamoja wakiwa katika msafara mkubwa wa magari 75.
Tofauti na namna ambavyo waliondoka Tripoli kuja Sirte ambapo waliondoka muda tofauti tofauti katika misafara midogo midogo.

Lakini safari hii waliondoka viongozi wakuu wote kwa pamoja na msafara mkubwa namna hii wa magari 75. Kwenye msafara huu alikuwemo Muammar Gaddafi mwenyewe, alikuwepo kiongozi mkuu wa jeshi Mansour Dhoa na waziri wa masuala ya ulinzi katika serikali ya Gaddafi, Abu-Bakr Yunus Jabr.

Kutokana na ukubwa wa msafara huu ulikuwa rahisi kuonekana hata kutokea angani.!
Wakiwa wamefika kama kilomita 3 nje ya mji wa Sirte, ndege isiyo na rubani (Predator Drone) ya jeshi la Marekani iliwang'amua na kuanza kuwashambulia.
Baadae ndege ya kivita ya jeshi la Ufaransa nayo ikaungana katika mashambulizi baada ya kitengo cha ushushushu wa kijeshi wa NATO kunasa mawasiliano ya simu ya Gaddafi na wasaidizi wake.

Gari ambalo alipanda Gaddafi halikushambuliwa moja kwa moja bali magari ya mbele yake ndiyo yalishambuliwa vibaya na kusababisha pia kupata ajali kwa gari ambalo Gaddafi alikuwa amepanda.

Shambulio hili la kwanza la NATO liliharibu kabisa magari yapatayo 20 na ikasababisha magari yapatayo kumi na moja kujitenga na msafara na kuendeshwa kwa spidi kubwa kukimbia kuelekea kusini mwa nchi.

Baada ya hapo likafuata shambulio la pili ambalo nalo liliharibu magari mengine zaidi ya 20 na kuvuruga kabisa msafara na muelekeo wake. Shambulio hili la pili pia lilisababisha wapiganaji wa ardhini wa NTC kukimbilia upande huu wa mji na kuanza kuushambulia msafara wa Gaddafi.

Kwa mujibu wa taarifa yao binafsi NATO wanadai kwamba hawakuwa wanajua kama Gaddafi yuko kwenye huu msafara Ila wao walishambulia ule msafara kama "military asset" ambayo walihisi ilikuwa na tishio.

Utetezi huu wanautoa ili kuogopa kuvunja kifungu cha kanuni ya mwaka 1973 cha Security Council Resolution. Kwamba NATO hairuhusiwi kulenga (targeting) mtu binafsi pali walenge "a military asset that pose a threat"!
Japokuwa baadae NATO ilikuja kukiri kwamba shambulio lao la anga lilichangia kwa kiasi kikubwa katika kukamatwa kwa Muammar Gaddafi.

Ikumbukwe kwamba mpaka muda huu Gaddafi bado alikuwa yuko hai.
Hivyo basi yeye pamoja na mwanae Mutassim Gaddafi na waziri wake wa ulinzi, Abu-Bakr Yunus Jabr walifanikiwa kutoroka kutoka kwenye msafara huu ulioshambuliwa vibaya kutoka angani na drone pamoja na ndege za kivita za NATO na bado ukiwa unaendelea kushambuliwa, wakatoroka na kwenda kujificga kwenye nyumba za karibu kutoka hapa walipokuwa.!


Wakiwa kwenye hiyo nyumba ya jirani waliyojificha wapiganaji wa NTC wakawashitukia walipo na kuzingira nyumba za jirani.
Majibizano ya risasi yakapamba moto kati ya walinzi wa Gaddafi na wapiganaji wa NTC.
Mutassim, yule mtoto wa Gaddafi akang'amua mapema kwamba hawawezi kujibizana kwa risasi na wenzao milele, muda si mrefu watazidiwa nguvu au kuishiwa risasi.
Hivyo basi akachukua walinzi wapatao ishirini na kutoka nje kwa njia ya kutambaa kwa tumbo lengo lao likiwa ni wafike barabarani ambapo msafara wao ulishambuliwa na kuangalia kama kuna gari lolote zima walitumie kumtoroshea Gaddafi.

Inaelezwa kwamba Mutassim alijitahidi sana kumsihi baba yake afuatane nao, na baada ya mabishano ya dakika kadhaa Gaddafi akakubali kwenda nao.

Wakatumia mtaro mdogo wa maji machafu unaopita eneo hilo la makazi 'kucrawl' ili wasiweze kuonekana.
Walifanikiwa kutambaa kwa tumbo kwenye mitaro hiyo mpaka kupata mkao mzuri wa "defensive position" ili waweze kujibu mapigo ya wapiganaji ya NTC.

Wakiwa hapa mtaroni moja ya walinzi wa Gaddafi alijaribu kurusha bomu la mkono kuelekea muelekeo walipo wapiganaji wa NTC lakini kwa bahati mbaya bomu hilo likagonga ukuta juu ya mtaro na kurudi pale pale walipokaa na kulipuka.
Mlipuko huu ulisababisha kifo cha yule mlinzi pamoja na waziri Abu-Bakr Yunus Jabr na Gaddafi alijeruhiwa vibaya sana.

Muda huu mtoto wake Mutassim alikuw a tayari ameelekea barabarani na wale walinzi 20.

Kwa hiyo licha ya kujeruhiwa vibaya sana Gaddafi na mlinzi wake ambao walibakia hai baada ya mlipuko walimbilia kwenye mtaro mwingine mkubwa zaidi ulijengwa kwa karavati.

Katika purukushani za kujiokoa kutoka pale mahali kwenye mtaro wa awali baada ya mlipuko, Gaddafi alikuwa amepigwa risasi mgongoni na alikuwa amejeruhiwa vibaya sana lakini bado alikuwa hai na anaweza kuongoa na kutembea kama kawaida.

Bado kuna utata ni namna gani wapiganaji wa NTC waliweza kung'amua mahali Gaddafi alikokimbilia kwa mara ya pili (kwenye mtaro mkubwa wa Karavati) lakini dakika kadhaa baadae wapiganaji hao walikuwa wamewasili eneo lilipo karavati.

Kuna baadhi ya wapinagaji wanadai kuwa walifuatilia michirizi ya damu iliyokuwa inamvuja Gaddafi lakini zipo ripoti zinazodai kwamba ni 'drone' ya Marekani ndiyo iliyo 'mtrack' Gaddafi mpaka kwenye mtaro alipokimbilia.

Vyovyote vile ukweli ulivyo, lakini uhalisia ni kwamba wapiganaji wa NTC walifika kwenye mtaro huu mkubwa na kupiga kelele kumuamuru Gaddafi atoke.

Pasipo kukaidi amri hii Gaddafi akatoka mtaroni akiwa amenyoosha mikono juu kwa ishara ya kujisalimisha. Nguo zake na mwili mzima alikuwa ameloa damu chapachapa.

Wapinagaji wa NTC wakalipuka kwa kelele za furaha na ushindi wakitamka kwa nguvu, "Muammar, Muammar, Muammar!!" na wengine wakipiga kelele za 'takbir', "Allah Akbar, Allah Akbar, Allah Akbar".


Gaddafi alikuwa ametiwa mikononi rasmi kwa maadui zake.

Baada ya kumtia mikononi tu, wapiganaji wa NTC ambao walikuwa katika hali ya furaha iliyopitiliza wakaanza kumshushia kipigo.
Baadhi ya wapiganaji wa NTC waliokuwepo eneo wa tukio wanadai kuwa Gaddafi alianza kuwaomba wasimuue na wasiendelee kumpiga. Alipoona vijana hao hawaelewi Gaddafi alitamka maneno kadhaa makali kama vile, "Mungu alaani hiki mnachokifanya", pia akawa anawauliza kwa kurudia rudia, " Mnajua tofauti ya jambo ovu na zuri?"

Lakini vijana hawa ilikuwa ni kama vile maruhani yamewapanda kichwani. Kitu pekee walichokiona mbele yao ni fursa ya kulipiza 'kisasi' ambacho labda hata hawakujua ni kisasi cha sababu ipi?

Yote haya waliyokuwa wanayafanya walikuwa wanayarekodi kwenye video kwa kutumia simu za mikononi.

Katika moja ya video hizo inaonekana moja ya wapiganaji akimuamuru Gaddafi asimame na Gaddafi akatii akijitahidi kusimama kwa taabu sana bila mafanikio.

Kwenye video nyingine wanaonekana wapiganaji hao wakifurahi kwa kupiga risasi hewani mfululizo na mpiganaji anamfanyia Gaddafi kitenfo cha ukatili mkubwa na udhalilishaji kwa kumchoma kisu/bayonet Gaddafi sehemu ya haja kubwa.

Bado kuna utata mkubwa ni muda gani hasa Gaddafi alifariki na aliuwawa vipi.
Kitu ambacho ni dhahiri ni kwamba alikamatwa akiwa hai. Lakini bado kuna swali alikufaje?

Iko video inayoonyesha akipandishwa kwenye gari la wagonjwa na hawa wapiganaji akiwa hai huku wanashangilia kwa kupiga risasi hewani.








Gaddafi mikononi mwa wauaji wake

Iko video nyingine inaonyesha mwili ambao ubaonekana dhahiri kabisa haukuwa hai ukiwa umelazwa kwenye gari la wazi.

Ripoti ya daktari baada ya mwili wake kufikishwa hospitali inaonyesha kwamba mwili ulikuwa na tundu la risasi kichwani.

Mwanzoni waasi walijitetea kwamba Gaddafi alikuwa kutokana na risasi kutoka kwa wanajeshi wake mwenyewe.
Yaani, wapiganaji hao walidai kwamba mara baada ya kumkamata Gaddafi wakiwa kwenye harakati za kumuondoa kutoka kwenye eneo walilomkamata na kumpeleka eneo la kumubifadhi, walishambuliwa ghafla na wanajeshi wanao muunga mkono Gaddafi na katika majibizano ya risasi, moja ya risasi kutoka upande wa wanajeshi wanaomuunga mkono Gaddafi ikampata kiongozi huyo kichwani na kupoteza maisha.

Lakini suala hilo halina ukweli wowote.

Uchunguzi wa kina uliofanyika baadae umegundua kwamba Gaddafi aliuwawa kwa kupiga risasi kichwani pamoja na wenzake wengine sitini na sita akiwemo mtoto wake Mutassim.

Kwa hiyo siku hii ya tarehe 20, mwezi October mwaka 2011, kiongozi wa Taifa la Libya, mtu ambaye alilitoa taifa hilo kutoka 'mavumbini' na kuliweka katika viwango vya juu kuwa moja ya nchi bora kabisa duniani, aliuwawa na raia wake mwenyewe kwa kusaidiwa na maafui zake wa miaka mingi wa magharibi, raia hao walio muua mdio hao hao ambao alitumia zaidi ya miongo minne kuwatumikia na kuwaletea maendeleo ya kihistoria.

October 20, 2011 ndio ilikuwa siku ya mwisho kwa Gaddafi juu ya uso wa dunia akiwa hai.

Kuna Vidokezo nimekuandalia vitakujia katika post zinazokuja kuhusu Makala hii.

Comments

Popular posts from this blog